Moduli hii ya Drama katika Elimu inakusudiwa kutalii nafasi ya drama kama nyenzo ya kufanikisha malengo mbalimbali ya elimu. Ieleweke kuwa elimu huweza kufasiliwa kama uwezo wa kukabiliana na hali mbalimbali ambazo mtu hukutana nazo katika maisha. Zaidi ya hivyo, tunazingatia pia kuwa malengo makuu ya elimu siyo maarifa bali vitendo. Hapa ndipo drama inapoonekana kuhitajika ili kufanikisha malengo makuu ya elimu. Hii ni kwa kuwa msingi mkuu wa usanaa katika drama ni vitendo. Kutokana na drama kuegemezwa katika vitendo, dhana ya drama katika moduli hii imetumika kwa maana pana kujumuisha aina zote za sanaa tendaji ambazo msingi wa uzuri wake wa kisanaa unajitokeza katika vitendo peke yake au vitendo pamoja na maneno.
Felician Nkwera (?) katika andiko lake la Tamrini za Fasihi, anatupatia msingi mzuri katika kuielewa maana ya sanaa na sanaa tendaji. Ijapokuwa katika aina zake tatu za sanaa tendaji (sanaa za vitendo, sanaa za maonesho, na sanaa za maumbo), tunakubaliana na aina mbili tu kuwa ndiyo zinafaa kuangukia katika sanaa tendaji. Aina hizi ni sanaa za vitendo pamoja na sanaa za maonesho, aidha, hatukubaliani na kutofautishwa kwa sanaa za vitendo na sanaa za maonesho kama alivyofanya Nkwera. Hii ni kwa kuwa zile anazoziita sanaa za vitendo na sanaa za maonesho zote kwa pamoja zinadhihirisha utendaji. Zaidi ya hivyo uzuri wake unajiokeza kupitia utendai/utendekaji. Hata mifano anayoitoa ya aina hizi mbili za inaonekana kuingiliana. Kwa mfano, matambiko, michezo ya watoto, jando na unyago inaonekana kujitokeza kwa aina zote mbili za sanaa. Hivyo katika moduli hii, aina hizi mbili za sanaa zinarejelewa kwa ujumla kama sanaa tendaji.
Mlaga (2017) anaeleza kuwa drama ni dhana pana ambayo ndani yake hujumuisha dhana mbalimbali zinazohusiana na uigizaji (maigizo). Katika maana hii ya jumla ndipo tunapokutana na aina mbalimbali za drama kama vile tamthilia, filamu, michezo ya runingani, michezo ya redioni, vichekesho, futuhi/komedi, utambaji hadithi, michezo ya watoto, Ngonjera, vibonzo jongefu, na jando na unyago kwa uchache. Katika mifano hii, tumezingatia kuwa kuna tanzu au vipera ambavyo ndani yake kuna udrama kwa maana ya kuwa kuna aina fulani ya uigizaji. Tanzu au vipera vyenye sifa hizi, huweza kuanishwa katika tanzu tofauti.
Wafula (2003) naye anaeleza kuwa "Katika kitabu hiki, neno drama litatumika kumaanisha somo linalohusu uigizaji wa hali fulani iwe ni vitendo au tabia au hisia za binadamu kwa kufuata taratibu maalumu." Katika maelezo haya yote mkazo upo katika vitendo. Hivyo basi kinachofanya drama ni kitendo kilichopo kwani mazungumzo peke yake hayafanyi drama.
Hivyo drama ni nyenzo muhimu sana katika kufanikisha malengo ya kielimu. Moduli hii inakusudiwa kuyadhihirisha haya yote kwa kujiegemeza katika aina mbalimbali za drama.